Pages

Sababu 7 za vibinti kushobokea penzi la watu wazima


Inakuwaje watu wangu? Natumaini kwamba mambo ni freshi na mnaendelea vyema na majukumu yenu ya kila siku. Mimi ni mzima bukheri wa afya na tunakutana tena kupitia safu hii, lengo ni kuwekana sawa katika masuala flaniflani yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi.

Ndugu zangu, hivi karibuni binti mmoja mwenye umri wa miaka 20 alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya jamii inayomzunguka kubaini kuwa anatoka kimapenzi na ‘mbaba’ mwenye umri zaidi ya miaka 55.
Wakati watu wakijiuliza inakuwaje mzee mzima kutoka na kibinti hicho, taarifa zikazagaa kuwa, si penzi la kawaida tu bali wawili hao wanatarajia kuoana hivi karibuni. Kweli Ijumaa iliyopita mzee huyo alimchukua ‘mtoto’ jumlajumla na sasa wanaishi kama mke na mume, watu wamebaki midomo wazi!
Lakini kila linalotokea lina sababu zake na kwa hili nimeona nilizungumzie leo. Uchunguzi unaonesha kwamba siku hizi vibinti vidogodogo vimecharukia sana mapenzi ya watu wazima.
Wapo ambao wanafikia hatua ya kuolewa na vijibabu vikiwemo vya kizungu, ukiuliza unaambiwa bora maisha huku wengine wakishadadia kuwa, vijana wa siku hizi ni pasua kichwa tu. Mapenzi yao yametawaliwa na usanii.
Huenda hayo yanayosemwa yana ukweli na yawezekana ndiyo maana leo hii tunaona kuna ndoa nyingi zinazofungwa huko mitaani kwetu ambazo anayeoa ni kama vile anamuoa mwanaye au mjukuu wake. Inashangaza sana!
Lakini kama umekuwa ukijiuliza kwa nini haya yanatokea, leo nitakupa sababu saba ambazo zinawafanya wasichana wadogo kuingia kwenye mapenzi na watu wazima na wengine kuolewa kabisa.
1. Wanajua kupatiliza wanawake
Katika uchunguzi uliofanyika kwa kuzungumza na baadhi ya wasichana, imeonesha kuwa wengi wao wanapapatikia watu wazima kwa kuwa wanajua namna ya kumpatiliza mwanamke. Wanajua kujali, kubembeleza na kuwafanyia wapenzi wao vitu ambavyo wanavitaka kwa wakati bila longolongo.
Inaelezwa kuwa, watu wazima wanawachukulia wapenzi wao kama watoto hivyo kuchukua nafasi ya kuhakikisha wanakuwa ni wenye furaha wakati wote.
2. Wanajua kuhudumia
Inasemekana kuwa, mtu mzima anapoingia kwenye uhusiano, anakuwa mwenye msimamo unaoweza kufanya mambo yakaenda kama alivyopanga. Akisema anakupenda anamaanisha kweli na atakuwa tayari kwa gharama yoyote kuhakikisha uhusiano au ndoa inadumu.
Linapokuja suala la fedha, watu wazima wanaonekana si wabahiri. Wanajua kuhudumia ili mradi tu wapewe penzi lenye ujazo unaostahili. Hapa ndipo panapowagusa wengi.
Katika wasichana 10 niliowauliza sababu za baadhi yao kupenda watu wazima, 9 walisema ‘wazee’ siyo bahiri na wanajua kuhudumia na kumfanya mwanamke aishi maisha ya raha mustarehe tofauti na vijana ambao mwanzo wanaweza kuanza kwa kujifanya wanajua kuhudumia lakini baadaye wanageuka kuwa ‘marioo’.
3. Wanajiamini
Asilimia kubwa ya wanawake ulimwenguni kote wanapenda kuwa na wapenzi/waume wenye msimamo na wanaojiamini. Hata hivyo inaonesha kuwa, watu wazima ni wenye msimamo na wanajiamini zaidi kuliko vijana na ndiyo sababu ya baadhi ya wasichana kuwashobokea.
4. Wamepevuka
Watu wazima ni watu waliopevuka kiakili na kimwili hivyo wana uwezo wa kuwafanya wapenzi wao nao wakapevuka kadiri siku zinavyokwenda. Ndiyo maana baadhi yao wakishaolewa au kuwa kimapenzi na watu wazima wanabadilika katika maamuzi. Hicho ni kitu kinachowafanya baadhi yao kupenda kuwa na watu wazima.
Itaendelea wiki ijayo.

No comments:

Post a Comment