Pages

FAINALI MISS UTALII TAIFA KUFANYIKA MWEZI HUU JIJINI DAR ES SALAAM


FAINALI za shindano la Miss Utalii Taifa, zinatarajiwa kufanyika Desemba mwaka huu jijini Dar es Salaam, imefahamika.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi katika Hoteli ya Ikondolelo iliyopo Kibamba, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Rais wa Kamati ya Miss Utalii Taifa, Gideon Chipungahelo ‘Chips’, alisema kuwa kambi ya taifa ya warembo watakaowania taji hilo, itafanyika katika hoteli hiyo.

“Ikondolelo Lodge ndiyo itakayokuwa hoteli maalum kwa ajili ya kambi ya mashindano ya Miss Utalii Tanzania, tumeamua kuweka kambi hapa kama sehemu ya kuitangaza hoteli hii inayomilikiwa na wazawa, Watanzania wenzetu, ikiwa ni miongoni mwa wadhamini,” alisema Chipungahelo.
Alisema kuwa warembo wapatao 60, wanatarajia kuanza kambi wiki hii, itakayokuwa ya siku zaidi ya 20, kujiandaa na shindano hilo.
“Kwa niaba ya Kamati ya Miss Utalii Taifa, ninapenda kuishukuru hoteli hii kwa kudhamini mashindano haya yanayolenga kuutangaza utalii wa Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuwahifadhi warembo zaidi ya 60 watakaokuwapo kambini kwa siku zaidi ya 20.
“Fainali za Miss Utalii Taifa mwaka huu, zitakuwa katika ubora wa hali ya juu na kuzidi mashindano yote yaliyofanyika miaka iliyopita, likiwamo lile la Dunia lililofanyika pale Ubungo Plaza.
“Katika fainali za mwaka huu, kutakuwa na tuzo tatu mbali ya taji la Miss Utalii ambazo ni tuzo ya Rushwa, Mazingira, Wanyama Pori, Hifadhi ya Bahari, Balozi wa Umasikini, Elimu ya Jamii, Afya ya Jamii, Utalii wa Kitamaduni, Utalii wa Michezo, Hoteli, Usafiri wa Anga na Usafiri wa Majini,” alifafanua Chipungahelo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hoteli ya Ikondolelo, Philip Humbie, alisema kuwa wapo bega kwa bega na Kamati ya Miss Utalii katika kufanikisha mashindano hayo na kwamba wameamua kujitosa katika mashindano hayo ili kuiunga mkono serikali katika juhudi zake za kutangaza utalii wa Tanzania.
“Lakini pia tumevutiwa na juhudi zinazofanywa na waandaaji wa mashindano haya, za kuhamasisha utalii wa ndani, utamaduni na utalii wa kimataifa. Tukiwa kama wawekezaji wazawa, tumeona tunalo jukumu la msingi kusaidia kutangaza utalii wa Tanzania, kwani sekta hiyo ni muhimu katika uchumi wa Tanzania,” alisema mkurugenzi huyo.
Alitoa wito kwa makampuni na watu bnafsi, hususan wawekezaji wazawa, kujitokeza kudhamini mashindano hayo.

No comments:

Post a Comment