FAMILIA ya Hussein Ramadhan Mkieti ‘Sharo Milionea’ aliyefariki dunia Novemba 26, mwaka huu kwa ajali ya gari iliyotokea Songa-Kibaoni, Muheza, Tanga imemteua msanii wa vichekesho Musa Kitale kuwa mwangalizi wa mali za marehemu, Amani limejuzwa.
Akizungumza na paparazi wetu jijini Dar hivi karibuni, Kitale alisema familia hiyo imemteua yeye kwa kigezo cha ukaribu wake na marehemu tangu zamani.
Alisema amepewa jukumu la kuhakikisha mikataba yote ambayo marehemu aliifanya na makampuni mbalimbali inakwenda vizuri sanjari na kuangalia mali kama vile gari na samani za ndani ya nyumba.
“Nimeambiwa nisimamie mikataba, niangalie mali za mshikaji (Sharo) kwa kipindi chote cha kusubiria arobaini ya marehemu ambayo itafanyika Januari 4, 2013 kijijini alikozikwa,” alisema Kitale.
Kitale alisema baadhi ya mikataba anaifahamu kwa vile yeye ndiye aliyekuwa shahidi, “lakini wa DTV aliosaini siku tano kabla ya kufariki dunia (hakuutaja) inabidi aushughulikie Muddy Suma jamaa aliyemuazima gari marehemu,” alisema.
Kuhusu kwenda kuzima taa katika nyumba aliyokuwa akiishi marehemu, Sinza Palestina Dar, Kitale alisema:
“Kwa kipindi hiki ambacho tunasubiri arobaini ya marehemu ifike ni ngumu mtu kwenda kufungua mlango ili azime taa, namuomba mama mwenye nyumba avumilie kwani zoezi la kufungua mlango wa kwa Sharo ni hadi familia yake iwepo hapa Dar na si mimi peke yangu.”
Akakumbuka jambo hili: “Tulishtushwa na taarifa tulizozisoma kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi iliyopita kuwa, kuna rafiki mmoja wa marehemu alikwenda pale nyumbani na kutaka kutapeli vitu vya marehemu, kama isingekuwa msimamo wa mwenye nyumba jamaa angefanikisha utapeli wake ndiyo maana haraka sana familia ikanipa mimi jukumu hili.”
No comments:
Post a Comment