MWANAMUZIKI wa muziki wa kizazi kipya nchini, Judith Wambura maarufu kwa jina la Lady Jay Dee, jana alifanikiwa kukamilisha ziara yake ya siku sita ya kupanda mlima Kilimanjaro, ikiwa na lengo la kutangaza mlima huo na kujionea upekee wa kivutio hicho.
Katika ziara hiyo iliyodhaminiwa na shirika la hifadhi za taifa nchini (TANAPA), msanii huyo aliyeambatana na mumewe ambaye ndiye anesimamia kazi zake, Gadna Habash, waliwasili kwenye lango kuu la Marangu saa
12 jioni na kupokelewa na mhifadhi mkuu wa hifadhi ya mlima Kilimanjaro (KINAPA), Erastus Lufungulo.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari mara baada ya kushuka mlimani, Jay Dee, alisema ziara hiyo imetoa mafunzo makubwa kwao na wakatoa wito kwa wasanii, waandishi wa habari na watangazaji nchini, kutembelea vivutio hivyo ili kufahamu yale wanayozungumza kuhusu hifadhi hizo.
“ziara hii imenipa mwanga kama msanii, nimejifunza mengi na niwakumbushe tu wasanii wenzangu kuchukulia zoezi la kupanda la kupanda mlima Kilimanjaro kama moja ya majukumu na wajibu wao kama wananchi wa taifa hili,” alisema Jide
Kwa upande wake mhifadhi wa KINAPA Lufungulo ametoa rai kwa wadau wote hasa wananchi wa kawaida kushiriki kupanda mlima huo, kwa lengo la kukuza utalii wa ndani.
No comments:
Post a Comment