Unywaji wa pombe ya ulanzi unadaiwa kuwa chanzo cha kuongezeka kwa maambukizi ya Ukimwi Iringa!!
"KARIBU mchumba, karibu unywe ulanzi, unataka mtogwa (uliogemwa leo) au mkangafu (wa siku nyingi)? Njoo ukae nami hapa usiogope! Mama Anita, lete lita moja fanya haraka mrembo asije akaondoka," hivyo ndivyo nilivyopokewa katika klabu cha pombe cha Ndiuka, Iringa.
"KARIBU mchumba, karibu unywe ulanzi, unataka mtogwa (uliogemwa leo) au mkangafu (wa siku nyingi)? Njoo ukae nami hapa usiogope! Mama Anita, lete lita moja fanya haraka mrembo asije akaondoka," hivyo ndivyo nilivyopokewa katika klabu cha pombe cha Ndiuka, Iringa.
Nilikwenda kufanyia kazi utafiti wa wataalamu unaosema kuwa moja ya sababu zinazochangia kasi ya maambukizi ya Ukimwi katika Mkoa wa Iringa ni ulevi hasa wa pombe za kienyeji.
Mmoja wa wauzaji wa pombe hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe anasema wakati wa msimu wa pombe ya ulanzi, wanywaji wengi hushindwa kuzuia tamaa zao za ngono na kujikuta wakijiingiza katika vitendo hivyo bila kinga."Ulanzi ukiwa mwingi ngono pia huwa nje nje! Ndiyo maana msimu wa ulanzi ukiisha tu wanawake wengi huwa na mimba zisizotarajiwa. Ulanzi ni hatari, unasababisha watu washindwe kujizuia na hatuwezi kuuacha kwani ni asili yetu," anasema.
Pombe hiyo iligunduliwa wakati wa utawala wa machifu wa kabila la Wabena katika Wilaya ya Njombe baada ya mti mchanga wa mwanzi kukatika na kuanza kutoa maji matamu.
Tangu wakati huo, pombe hiyo imekuwa ikithaminiwa na wakazi wa Mkoa wa Iringa na tayari imeshambaa na kufika katika maeneo mengine mengi hasa kusini mwa Tanzania.
Wanywaji wengi wa ulanzi wanasema bila shaka kwamba pombe hiyo inachangia kasi ya Ukimwi.
"Msimu wa ulanzi huwa unauzwa bei rahisi ambayo hakuna inayemshinda ndo maana watu wengi hulewa hivyo kuwa rahisi kwao kufanya ngono bila kujiandaa kwani wanawake wengi wakishanunuliwa kinywaji hicho huwa wepesi kukubali," anasema Richard Mwenda.
Mtaalamu wa magonjwa ya ngono mkoani Iringa, Dk Paul Luvanda anasema pombe hiyo ndiyo kichocheo kikubwa cha ngono zembe hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa maambukizi ya Ukimwi.
"Ulevi hasa wa pombe ya ulanzi unachangia kuongeza hamu ya kufanya ngono zembe, wengi wamejikuta wakipata maambukizi kutoka na pombe hii ambayo inaheshimiwa na wenyeji," anasema Dk Luvanda.
Ulanzi siyo kichocheo pekee, Luvanda anataja mila na desturi potofu ambazo jamii nyingi mkoani humo bado inaziendeleza. Miongoni mwazo ni kurithi wajane, kukosekana kwa usawa kijinsia, kutakasa wajane na wasichana, kuoa wake wengi, imani za kishirikina na kutotahiri.
Nyingine ni umaskini wa kipato. Maisha ya wananchi wengi ni duni.
Anasema kutobadili tabia licha ya elimu ya ukimwi kuwafikia wananchi na wengine kuathiriwa kwa njia moja au nyingine na Ukimwi ni miongoni mwa sababu za kuenea kwa ugonjwa huo.
Anataja sababu nyingine kuwa ni muingiliano mkubwa wa watu kutokana na shughuli nyingi za biashara na ongezeko la taasisi mbalimbali mkoani humo.
Hali ya maambukizi ikoje?
Dk Luvanda anasema watu 17,555 kati ya 71,628 waliojitokeza kupima kwa hiari kati ya Julai 2008 hadi Juni 2009, walikutwa na maambukizi ya VVU. Hali inayoonyesha kwamba maambukizi yameongezeka na kufikia asilimia 24.5 hali ambayo ni hatari.
Anasema kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa hali ya ukimwi kitaifa mwaka 2003/2004, maambukizi yalikuwa asilimia 13.4 na mwaka 2007/2008 yakapanda na kufikia asilimia 15.7.
"Utafiti unaonyesha Iringa tupo asilimia 24.5, hii siyo hali ya kawaida hata kidogo." Anasema Wilaya ya Makete inaongoza kwa kuwa na asilimia 35.9, Njombe 31.9, Iringa 30.5, Mufindi 24.0, Manispaa 23.5, Ludewa 18.6, Njombe mjini 21.1 na Kilolo 12.2.
Hadi Juni 2009, wananchi walioandikishwa kweny mpango wa dawa za kupunguza makali ni 51,137 na walioanza kutumia dawa hizo ni 25,703.
Wakati maambukizi ya Ukimwi mkoani Iringa yakiongezeka kwa kasi, takwimu za kitaifa zinaonyesha kuwa yamepungua kutoka asilimia saba mwaka 2003 hadi asilimia 5.8 mwaka 2007.
Hiyo ina maana kwamba Mkoa wa Iringa ndiyo wa kwanza nchini kwa kuwa na kiwango cha juu kabisa cha maambukizi, ukifuatiwa na Dar es Salaam yenye asilimia 8.9 na wa tatu ni Mbeya yenye asilimia 7.9.
Kutokana na kiwango hicho cha maambukizi mkoa unakisiwa kuwa na watu 246,935 wanaoishi na VVU/Ukimwi kati ya wakazi wake wote zaidi ya milioni 1.5 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002.
Idadi ya watoto yatima nayo imekuwa ikiongezeka siku hadi siku kutokana na wazazi wengi kupoteza maisha. Watoto 67,915 wameshatambuliwa na 30,303 wanapatiwa misaada ya chakula, mavazi, malazi na elimu.
Mkoa unafanya nini?
Kupaa kwa takwimu za maambukizi ya Ukimwi kunaonyesha kuwa jitihada mbalimbali zinazofanywa na mkoa huo kupambana na janga hilo zimegonga mwamba.
Hata hivyo, Dk Luvanda anasema umeandaa mkakati wa kupambana na kasi hiyo ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2008 utakaomilika Septemba 2012 ukilenga kupunguza kasi hiyo kwa asilimia 50.
Anasema tayari Sh1.8 bilioni zimeshatumika kuanzia Juni 2008 hadi June 2009. Kati ya fedha zilizotumika, Sh953.9milioni ni kutoka serikali kuu wakati Sh870.1milioni ni michango wa wadau mbalimbali wanaoshiriki katika mapambano ya Ukimwi Iringa.
Dk Luvanda anasema Wilaya ya Makete ilitumia Sh 942.5milioni, Ludewa 150.7milioni, Manispaa 22.2 milioni, Iringa Vijijini 116.2 milioni, Kilolo 54.6 milioni, Mufindi 442.6 milioni na Wilaya ya Njombe ilitumia Sh114.8 milioni.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Ezekiel Mpuya anasema mkakati huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mapambano dhidi ya Ukimwi katika halmashauri za wilaya na kuwa umeandaliwa kwa kuzingatia vipengele vilivyomo katika Mkakati wa Pili wa Taifa wa Mapambano ya Ukimwi (NMSF) wa mwaka 2008 hadi 2012.
Mpuya anasema mpango huo umezingatia pia ushirikishwaji wa wadau mbalimbali walio katika mapambano ya Ukimwi mkoani Iringa, pamoja na maelekezo ya wataalamu wa ndani ya mkoa na taifa.
Anasema mipango iliyoibuliwa inatekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja mmoja na kutathminiwa kila mwaka kisha kuendelezwa na mipya kuibuliwa kulingana na matokeo ya tathmini.
Anasema huduma za tiba zinatolewa katika hospitali 16 zilizopo mkoani Iringa na vituo vya afya 14 kati ya 26. Lengo ni kufikia vituo vya vyote.
Ili kufikia lengo hilo, mkoa unatekeleza mikakati minne ambayo ni pamoja na kutoa huduma za majumbani kwa wagonjwa wa Ukimwi, tiba na huduma muhimu kwa wagonjwa wa Ukimwi na watu wanaoishi na VVU, kuanzisha mapambano dhidi ya Ukimwi sehemu za kazi katika sekta ya afya na kutoa misaada mbalimbali kwa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mohamed Abdulaziz anatilia shaka takwimu hizo. Anawataka wataalamu kukaa upya na kuzitafiti ili kujua kama kweli ni hali halisi.
“Pamoja na mikakati yetu, wataalamu kaeni mfanye utafiti upya tujue kama kweli hizi ndizo takwimu au siyo na kama ni kweli, kuna kila sababu ya kutangaza hali ya hatari kwa mkoa huu,†anasema
Wananchi wanasemaje?
Wakazi wengi wa Mkoa wa Iringa wanataka mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea kutoa elimu ya ukimwi na kuhakikisha kuwa misaada na fedha zinazotolewa kwa ajili ya janga hilo zinawafikia walengwa.
Lakini wanashangazwa na kitu kimoja. Ikiwa wengi wanalalamikiwa kwa kufanya ngono zembe baadhi ya maeneo hayana kondom na mengine watalaamu hawajawaeleza kinagaubaga juu ya matumuzi na umuhimu wake
0 comments :
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !