Wajawazito wanywaji pombe kuzaa watoto taahira! - HABARI ZA MPEKUZI BLOG, BOSS NGASSA, RAHATUPU BLOG AND BONGOCLANTZ
Headlines News :
Home » » Wajawazito wanywaji pombe kuzaa watoto taahira!

Wajawazito wanywaji pombe kuzaa watoto taahira!


MATOKEO ya utafiti mpya umeonyesha kuwa matumizi ya pombe kwa wajawazito husababisha watoto kuzaliwa wakiwa na uwezo mdogo wa akili (utaahira).
Hayo yamebainishwa wakati kukiwa na mitazamo tofauti kuhusu matumizi ya pombe wakati wa ujauzito.

Utafiti huo uliofanywa na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha nchini Marekani (CDC), unaonyesha kuwa matumizi ya pombe kwa mjauzito ni hatari na hayafai.

Utafiti huo ulihusisha pia takwimu za miaka minne za kuanzia 2006 hadi 2010 nchini humo na kuchapishwa na Jarida la Afya la HHS Health Beat la nchini humo.
Mtafiti kutoka CDC, Claire Marchetta alisema kuwa utumiaji wa pombe wakati wa ujauzito huleta madhara ya kudumu kwa mtoto; kimaumbile hata kiakili.
Marchetta alisema: “Madhara hayo yanaweza kuwa ya kimaumbile kama vile kutokukua vizuri, matatizo ya moyo, figo au mifupa na yanaweza pia kusababisha matatizo ya kitabia.
Alifafanua kuwa matatizo ya kitabia alisema ni pamoja na kuwa na ufahamu mdogo na maradhi yanayosababisha mtoto kukosa umakini.
Alibainisha kuwa, hakuna aina yoyote ya pombe iliyothibitika kuwa ni salama kwa mjamzito.
Kumekuwa na mitazamo tofauti nchini kuhusu matumizi ya pombe wakati wa ujauzito, huku wengine wakisema kiasi kidogo cha pombe ni kizuri kwa mjamzito kwa madai kuwa kinasaidia kumwongezea damu mjamzito na kumchangamsha mtoto tumboni.

Utafiti huo umeonyesha kuwa katika kipindi hicho cha miaka minne, zaidi ya nusu ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 44, wanatumia pombe kila siku, huku asilimia nane ya idadi hiyo wakiwa ni wajawazito.
Mkazi mmoja wa Sinza, jijini Dar es Salaam ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa, alipokuwa mjamzito mama yake alimshauri kutumia pombe kiasi kwa maelezo kwamba ingesaidia kumchangamsha mtoto aliyekuwa tumboni.
Hata hivyo alisema kuwa, hakufuata ushauri huo wa kunywa pombe baada kushauriwa na daktari kutofanya hivyo kwa sababu ina madhara kwa afya ya mtoto aliye tumboni.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Aga Khan ya jijini Dar es Salaam, Dk Munawar Kaguta alibainisha kuwa, kiafya si sahihi kwa mwanamke mjamzito kutumia pombe, kutokana na ukweli kwamba, anaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa afya ya mtoto wake.

Aliongeza kuwa tatizo la wanawake wajawazito kunywa pombe lipo nchini, ingawa siyo kubwa kama lilivyo kwa nchi za nje.
Dk Kaguta alisema kuwa hajawahi kukutana na mwanamke ambaye amejifungua mtoto mwenye mtindio wa ubongo kwa sababu ya unywaji wa pombe ingawa yapo madhara mengine.
“Kwa hapa Tanzania sijawahi kukutana na tatizo hilo ingawa ni sahihi kabisa kwamba kuna uwezekano mkubwa mtoto kudhurika ikiwa mama mjamzito atatumia pombe kupita kiasi,”alisema Dk Kaguta.
Alisema kuwa asilimia kubwa ya wajawazito anaowahudumia wameelimika, hali inayomfanya ahisi kuwa wanawake wanaanza kuchukua hatua za kujizuia kunywa pombe wakati wa ujauzito.

Mtoto anavyoathiriwa
Kwa mujibu wa taarifa za kitabibu kutoka Mtandao wa Habari za Afya wa Tanzmed, unapokunywa pombe huingia moja kwa moja kwenye mzunguko wa damu wa mama, kisha hufika kwa mtoto kwa kupitia kondo la nyuma.

Pombe inapoingia kwenye mzunguko wa damu wa mtoto, huathiri uwezo wake wa kupata chakula, virutubisho na hewa ya Oksijeni ya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya kawaida katika ubongo na viungo vingine.
Hali hiyo inaelezwa kitaalamu kuwa inaweza kuathiri ubongo wa mtoto na ukuaji wa viungo vya mwili kwa jumla.
Dk Colin Carter, Mkufunzi wa madaktari wa watoto katika Shule ya Utabibu ya Harvad, anasema kuwa mtoto ambaye mama yake alikuwa akitumia pombe wakati wa ujauzito, hupata matatizo ya kuongezeka uzito tangu akiwa mchanga hadi atakapofikisha miaka tisa.

Dk Carter ambaye ametoa kitabu kinachohusu masuala ya afya ya mama na mtoto cha ‘Alcoholism: Clinical &Experimental Research’ anasema kuwa madhara atakayopata mtoto ni ya kudumu na yanaweza kuathiri uwezo wake wa ukuaji wa akili.
Utafiti mwingine uliofanywa nchini Afrika Kusini na kuhusisha wanawake 148 waliogawanywa katika makundi mawili ulibainisha kuwa, watoto ambao wazazi wao walikuwa wakitumia pombe, walikuwa na matatizo ya ukuaji, uzito na kuwa na vichwa vidogo.
Katika utafiti huo, wanawake hao waligawanywa katika makundi mawili; kundi la kwanza la wanawake 85 walikuwa wakitumia pombe zaidi ya mara moja kwa siku na lingine la wanawake 63 ambao hawakuwa wakitumia pombe kabisa.
Baada ya kujifungua, watoto wao walipofikisha miezi sita na nusu hadi mwaka mmoja walifanyiwa uchunguzi, ambapo watoto wa waliokuwa wakitumia pombe walikuwa na matatizo hayo.
Madhara mengine ya pombe kwa mtoto ni pamoja na kuzaliwa akiwa na uzito mdogo, ulemavu wa mbavu na kidari, matatizo ya mgongo uliopinda (kibiongo) na vidole vilivyoungana.
Pia mtoto anaweza kuzaliwa akiwa na kichwa kidogo kuliko kawaida, matatizo ya pua, taya na kutokuona mbali.
Share this article :

0 comments :

Speak up your mind

Tell us what you're thinking... !

Random Post

ARUSHA
 
Template Design by Creating Website Published by Mas Template