Pages

Siri 20 usizozijua za kufurahia mapenzi! - 5


FURAHA yangu ni kuona marafiki zangu wote mpo wazima na mchakamchaka wa maisha unaendelea kama kawaida. Sina shaka wengi mmekuwa mkivuna mambo mengi mazuri kupitia safu hii na maisha yanaendelea kuwa mazuri.

Leo tunahitimisha mada hii ambayo imedumu hapa kwa wiki tano – ni muda mrefu hakika, lakini wenye manufaa na kuongeza kitu kipya katika maisha yetu ya uhusiano.
Nazungumzia juu ya siri 20 ambazo kama zikitumika kikamilifu katika uhusiano, basi suala la mateso ya mapenzi litabaki kuwa simulizi za kusisimua. Tumeshaona siri kumi na nne za awali, ambazo zinawahusu zaidi wale ambao wapo katika hatua ya urafiki na uchumba.
Aidha, wiki jana niliingia katika siri nyingine sita kwenye kipengele cha pili, kinachowahusu wanandoa. Katika eneo hilo nilitaja siri tatu ambazo ni kuweka mipango pamoja, kutumia majadiliano katika kutatua migogoro na namna ya kupalilia ndoa.
Sasa leo tunamalizia vipengelea vitatu vya mwisho. Twendeni darasani rafiki zangu.

18. KINYWA CHENYE LADHA
Inawezekana ukaona labda nazungumzia kitu cha kawaida sana, lakini kama ukitafakari kwa kina na kwa mapana yake, utagundua kwamba ni mjadala wenye maana katika ndoa.
Hata kwenye Kitchen Party, sherehe za ndoa n.k, suala la kinywa chenye ladha nzuri huzungumzwa sana, ila hapa nitakuongezea baadhi ya vitu vingine usivyovijua.
Kwa kawaida, wanawake ndiyo ambao huaswa zaidi katika kuwa na kauli nzuri kwa waume zao. Wanaume wamesahaulika kabisa. Wanaonekana kama wao hawana wajibu wa kuwa na kauli nzuri kwa wake zao; jambo hili si la kweli hata kidogo.
Wote wanapaswa kuweka masikilizano kwa kauli ya pamoja, huku kila mmoja akiwa na shabaha ya kuhakikisha mwenzake haudhiki na maneno yake. Ni jambo jepesi sana – kuwa na ulimi wenye ladha.

KUJITAMBUA kwamba unayezungumza naye ni mke/mumeo. Hebu jiulize, ikiwa mwanzoni wakati wa uchumba wenu mliweza kuwa na kauli nzuri, kila mmoja akiwa na hamu ya kumsikiliza mwenzake muda wote, iweje katika ndoa?
Jibu la swali hili litakuwa mwongozo mzuri zaidi wa kuinakshi ndoa yenu kuwa bora yenye furaha siku zote. Ndugu zangu, furaha ndiyo kila kitu katika uhusiano wowote ule. Kukiwa na furaha, hakuwezi kuingia tatizo lolote. Litapitia wapi, wakati mioyo ina amani?
Ikiwa kinyume chake, ni rahisi hata kugombana, maana hata mgombanishi hupata nafasi zaidi sehemu isiyo na amani, isiyo na majadiliano, pasipo na maelewano. Usikubali kuwa katika ndoa ya namna hiyo.

19. EPUKA MANENO YA KUUDHI
Kipengele hiki hakina tofauti sana na kilichopita, lakini hapa kuna la zaidi la kuongezea. Kuna wakati wenzi wanaweza kuingia katika mtafaruku ambao chanzo chake ni cha ajabu kabisa! Kwa mfano, unakuta mpenzi anamwambia mwenzake: “Mh! Na wewe unanuka sana mdomo!”
Kauli gani hiyo kwa mpenzi wako? Mwanaume unalala naye kila siku, kwa nini umwambie ananuka? Wewe ukifanya hivyo, huko nje wamuambieje? Kwanza kama ni kweli ana tatizo hilo, ni jukumu lako kumtibu, lakini pia kumtunzia siri.
Kama nje anachekwa, ndani ya familia pia anachekwa, wapi atapata faraja? Yapo maneno mengi sana yenye kuudhi, lakini hapa nitataja machache. Wengine wanawaambia wenzao wananuka kikwapa, hawajapendeza, hawana akili nk.
Haya ni maneno ya kuudhi. Hebu fikiria kauli kama hii mtu anamtamkia mkewe! “Yaani kweli wewe huna akili, kitu kidogo kama hicho kweli unaweza kukosea? Ndiyo maana wenzetu wanafanikiwa kimaisha, wanatuacha. Sijui nilikutana na wewe wapi?...maisha yangu yanazidi kuwa giza tu, nikiwa na wewe!”
Acha maneno ya kufuru, kwani siku zote hukuona upungufu wake? Kuwa makini na kauli zako. Ndoa yako utaivunja wewe mwenyewe, pia kama ni kuijenga, utaijenga wewe mwenyewe!

20. UBORA KATIKA TENDO LA NDOA
Hapa ndipo panapotakiwa kupewa heshima kubwa zaidi kuliko vipengele vyote vilivyotangulia. Katika masomo yaliyopita, nimewahi kufafanua hili kwa undani zaidi, leo nitagusia juu juu tu!
Rafiki zangu, tendo la ndoa ni la heshima. Halitaki papara na linatakiwa kupewa nafasi na kila mmoja kuridhika. Acha kujifikiria mwenyewe, maana hapa ndipo panapopatikana mianya ya kutoka nje ya ndoa.
Hakikisha mwenzako anaridhishwa na wewe mnapokuwa chumbani. Tafuta elimu zaidi ya kufurahia tendo hilo ili mwenzako awe na sababu ya kuwa na wewe. Sikia nikuambie, tendo la ndoa kwa wanandoa hasa waliozoeana linachosha!
Huu ni ukweli ambao wengi wanaupinga. Yes! Linachosha na kukikanaisha. Hakuna kipya. Mwanaume yule yule. Kitanda kile kile, chumba kile kile. Lazima umchoke.
Hata hivyo, ukiwa mbunifu utaendelea kumuona mwenzako mpya kila siku. Badilisheni mazingira, tafuteni muda wa kutoka pamoja angalau mara moja ndani ya miezi mitatu – kwa mwaka mara nne.
Yapo mengi sana, elimu hii ni pana, hasa kama utakuwa mbunifu na mwenye kuisaka kila siku. Rafiki zangu, nadhani mnafahamu namna inavyokuwa vigumu kueleza kila kitu hapa gazetini, lakini kikubwa cha kumalizia mada hii ni hiki; unapokuwa na mwenzako faragha, ujue kuwa anategemea zaidi wewe kumfanya afurahie tendo hilo.
Ukijua hivyo, naye akajua hivyo, furaha ya tendo la ndoa itadumu siku zote za ndoa yenu. Nina imani unakwenda kutengeneza ndoa imara, bora ambayo itadumu, maana wewe ni mdau wa All About Love na umesoma mada hii na kuielewa. Ahsante kwa kunisoma.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na Who is your Valentine?, vilivyopo mitaaani.

No comments:

Post a Comment