Sehemu ya ukuta iliyobomoka na kusababisha kifo cha mwanafunzi mmoja.
Wasamaria wema wakijaribu kumwokoa kijana aliyeangukiwa na ukuta kwa kufukua kifusi kwa mikono.
MWANAFUNZI wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Kwakilosa  katika Manispaa ya Iringa Daniel Yona (15) amefariki dunia baada ya  kuaungukiwa na ukuta wa uwanja wa Samora wakati akijaribu kupita mlango  wa panya ili kwenda kushuhudia tamasha la Mtikisiko 2012.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Desemba 2 mwaka huu wakati  wapenda burudani katika mkoa wa Iringa walipofika katika uwanja huo  kushuhudia onyesho kubwa la Mtikisiko 2012 ambalo lilikuwa limepambwa na  wasanii mbali mbali wakiongozwa na mkongwe Juma Nature na Profesa J.
Wakielezea kilichomkuta mwanafunzi huyo baada ya mashuhuda walisema  kuwa mwanafunzi huyo na wenzake waliacha kupita katika mlango wa  kawaida kwa kulipia kiingilio halali kilichowekwa na badala yake aliamua  kupita gizani na kupanda ukuta huo wa uwanja wa Samora ili kuweza  kuingia ndani ya uwanja huo kuona tamasha la Mtikisiko.
Hata hivyo mmoja kati ya mashuhuda ambae hakupenda kutajwa jina  lake hapa alisema kuwa kabla ya mwanafunzi huyo kupanda ukuta huo kuna  vijana kama 20 ambao walifanikiwa kupita eneo hilo bila kulipa kiingilio  na baada ya kufanikiwa kupita walianza kupigiana simu huku baadhi ya  vijana wa kitanzini wakiwatoza vijana hao wanaoruka ukuta kiingilia cha  shilingi 1000 hadi shilingi 500 .
"Ujue hapa vijana wa kihuni kutoka Kitanzini walikuwa wamejipanga  hapa na kufanya ufisadi wa kuwatoza watu kiingilio bila wahusika wa  Tamasha hilo kujua kinachoendelea .....hivyo hata huyo mwanafunzi  alikuwa ni mmoja kati ya wavamizi wa Tamasha hilo kwa kupita njia ya  panya ili kuingia ndani ya uwanja huo"
Pia alisema ukuta huo ulionyesha kuzidiwa nguvu kutokana na ubovu  wa ukuta wenyewe kuwa ni mbovu na ulikuwa umeungwa kienyeji katika eneo  hilo.
Aidha alisema baada ya vijana zaidi ya watano kupanda eneo hilo la  ukuta ambalo lipo upande wa kushoto mwa uwanja huo wa uwanja ukuta huo  ulionyesha kuyumba na kupelekea vijana wengine kuruka na kumwacha  mwanafunzi huyo ambae tayari alikuwa ameingiza mguu mmoja ndani ya  uwanja na mguu wa pili ulikuwa nje. 
Alisema baada ya ukuta huo kuanguka na kumfunika walifanikiwa  kumwokoa akiwa hai na kumkimbiza Hospitali ya mkoa wa Iringa ambako  asubuhi ya siku ya pili ya Desemba 2 majira ya saa 5 asubuhi alifariki  dunia.
Hata hivyo askari polisi waliokuwepo eneo hilo la tukio  walimthibitishia mwandishi wa mtandao huu kuwa ni kweli kijana huyo  amefariki dunia japo wao si wasemaji wa jeshi la polisi na kudai kuwa  chanzo ni kijana huyo mwenyewe kutaka kupita mlango wa panya na kuacha  kupita mlangoni ambako watu wote walikuwa wakipita bila kupata matatizo  yoyote.
Hata hivyo uchunguzi wa mtandao huu unaonyesha kuwa kifo cha  mwanafunzi huyo kimesababishwa na mwanafunzi mwenyewe kutokana na kutaka  kupita njia ya panya na kuacha mlango kwani iwapo angetumia njia sahihi  kuingia uwanjani yawezekana kifo kisingeweza kutokea
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
0 comments :
Speak up your mind
Tell us what you're thinking... !